Je unafahamu juu ya athari za “BakoBako” TANZANIA...SEHEMU YA KWANZA


                                                                      
Na Alicia Evance.
Maendeleo katika sekta ya sayansi na teknolojia ni moja ya harakati katika nchi za Afrika na imeweza kuinua sekta ya mawasiliano.
Katika moja ya matunda ya harakati hizi jamii ya watu wa Afrika hasa Tanzania imeweza kubadili mfumo wa mawasiliano kutoka analojia kwenda digitali, ingawa ilikuwa ni harakati ngumu kufanikisha lakini Tanzania imeweza kupiga hatua na kuwa katika hadhi moja na nchi zingine za Afrika na hata bara la Ulaya.
Kwa kipindi cha miaka mitano ya digitali jamii imepokea maingizo tofauti ya simu kwa ajili ya mawasiliano, lakini toleo hili la simu aina ya ‘bakobako’ limepokelewa kwa kiasi kikubwa na jamii hasa vijana kuliko toleo zilizotangulia.
BakoBako yaweza kuwa sio jina sahihi lakini ni maana moja na majina tofauti kwa simu za mkononi yaani“smartphone” na hii ni kutokana na tofauti ya upokeaji wa simu hizi katika jamii, lakini pamoja na majina hayo tofauti jina la BakoBako limeenea sana katika kanda zote za Tanzania.
Takwimu zilizofanywa na vituo mbalimbali kama Pew research center tangu mwaka 2014 zinathibitisha matumizi ya simu aina BakoBako hasa kwa vijana kuliko simu za kawaida kama nokia tochi na mnara.
Kutokana na utafiti huo imetambulika kuwa asilimia 70 ya watu katika jamii wanaotumia simu za aina hii ni vijana na ni asilimia 30 ya wanajamii waliosalia wanatumia simu za kawaida, ikiwa asilimia 20 kati ya 30 ni wanawake wenye kipato cha chini na asilimia 10 iliyobaki ni wanaume wenye hali kama hiyo.
 Uchunguzi unaonesha kuwa, kati ya asilimia 70 ya vijana wanaotumia aina hii ya simu huegemeza matumizi yao na kutumia muda mwingi katika kutuma ujumbe mfupi kuliko kufanya mambo ya kimaendeleo na wengi wao kutumia simu hizo katika mitandao ya kijamii ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili katika jamii kama inavyoonyesha katika jedwali.
            

“BakoBako zinamatumizi tofauti kwa watu tofauti, lakini kutuma ujumbe, kuchukua picha na video na kuingia katika mitandao ya kijamii ndio matumizi makubwa yanayofanywa na asilimia kubwa ya vijana wanaomiliki simu hizi”
Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba vijana hupoteza muda pamoja na pesa kwa kufanya mambo yasiyo ya maendeleo katika simu zao na hivyo kuleta hasara kubwa katika jamii.
“Pamoja na takwimu hizi za matumizi ya simu, jamii na wanaharakati hawajapambanua bado fikra zao, kwanini vijana pekee ndiyo wanaoharibika? Kwani hapo kabla kijana wa miaka 15 hakuruhusiwa kumiliki simu lakini hii leo mtoto wa miaka 12 anayejiita kijana anamiliki simu ambayo hata mimi sijawahi kumiliki” alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Khamis (35).
Pengine maneno ya Khamisi yanaweza yasifuatiliwe lakini ni jambo gani hasa mtoto wa miaka 12 anajifunza katika simu?  ni kama mtindo sasa vijana kupiga picha za utupu na kuweka mitandaoni, kusambaza video ambazo hazina mafunzo kwa jamii na pia kutuma ujumbe usio na maadili, kwa hili mtoto huyu wa miaka 12 anajifunza nini.
Tanzania haina budi kujilaumu lakini jamii itazame jambo hili kwa darubini ndani ya bahari, kumruhusu kijana au mtoto wa miaka 12 kumiliki simu aina ya Bakobako kumfungulia akaunti na pengine hufungua mwenyewe katika mitandao yote ya kijamii na kujiunga na makundi tofauti bila kujua mipaka yake kwa umri huo anatakiwa kuishia wapi katika elimu ya dunia.
Bi.Rozalia anatazama jambo hili kwa upevu wake, akiwa ni miongoni mwa watu wanaotumia bakobako anasema “vijana wanaamini kwamba ni wakati wa mapinduzi ya utandawazi, wanatakiwa kujua kila kitu mzee anachojua, wanaamini kwamba kijana hafunzwi na jamii bali simu inamfunza kila kitu”.
Maneneo haya yaweza kuwa kweli kwani asilimia kubwa ya masomo hufundishwa; “google, wikipedia, youtube na browser”, hili pengine pia huwapa kiburi vijana lakini, yale wanayojifunza huko sio sahihi kwa muda wao kujifunza, kama kijana anajifunza kila kitu katika mitandao kuna haja gani ya msemo, asiyefunzwa na mamaye ulimwengu utamfunza?
Vijana kama nguvu kazi ya taifa wanatakiwa kuwa mfano katika matumizi bora ya simu zao, kijana wa miaka 13 hadi 17 anatumia BakoBako kwa ajili ya mitandao ya kijamii inamsaidia nini? ingawa mjadala utarudi palepale lakini suluhisho ni kuweka umri sahihi wa kijana kuanza kumiliki simu na kumiliki akaunti zake katika mitandao, lakini ni wangapi wataunga mkono jambo hili?
Kijana anatakiwa kufahamu matumizi sahihi ya simu kulingana na umri na wakati wake wa kujifunza na kutambua mambo kwa undani na kwa manufaa zaidi kuliko kupoteza pesa kununua vocha na muda mwingi kwa ajili ya picha, video na ujumbe usiokuwa na manufaa na hivyo atumie muda huo kwa ajili ya kutafuta njia ya kuleta maendeleo katika jamii.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment