Na Alicia Evance.
Unawezaje kuuishi uanamke wa zamani wakati wewe ni
msomi? ni kwanini unafanya shughuli zote za ndani na umeelimika? unawezaje
kuishi maisha ya dhiki ili kumtumikia mwanaume aliyekuoa wakati wewe mwanamke
ni msomi?
Niliyapanga vizuri maswali haya wakati nilipopatiwa
nafasi ya kuendesha mjadala uliopangwa kuhudhuriwa na wanawake wasomi ambao
baadhi yao ni wanawake wenye hadhi kubwa na heshima pia hapa nchini.
Ingawa mjadala haukufanyika kama ulivyotakiwa lakini
kuna kitu nilijifunza kutoka katika maandalizi ya mjadala huu, timu nzima ya
maandalizi ilinifunza jambo juu ya fadhila ya usomi kwa mwanamke na thamani
yake kwa jamii.
Ni takribani miaka 41 tangu elimu ya jinsia na usawa
ianzishwe nchini Tanzania lakini ni asilimia 60 tu ya wanawake waliofanikiwa
mpaka hii leo ingawa bado jitihada zipo zakufanikisha maendeleo kwa mwanake
nchini lakini, serikali inaangalia madhara ya elimu hiyo kwa mwanamke? Je
mwanamke anatambua lengo la serikali kumpatia kipaumbele katika elimu?
Mjadala uliofanyika mwaka 2012, septemba na taasisi ya
wanawake na maendeleo(WAMA), mama Salma Kikwete akiwa ni mwenyekiti wa taasisi
hiyo alieleza faida ya elimu kwa mwanamke kwamba, ni kwa ajili ya kumuwezesha
mwanamke kupambanua matatizo yaliyopo katika jamii ikiwa ni pamoja na ujinga,
magonjwa na umaskini na siyo kupindua jamii yake.
Hili ni jambo la kipekee sana na yapaswa mtu kufurahi
na kushukuru unapozaliwa mwanamke, si kwamba wanaume hawana thamani kwa jamii
la hasha, mwanamke amekuwa akitazamwa kama mboni angavu kwa karne zaidi ya
kumi.
Bi. Edna Henry ni mjasiriamali na ni mhitimu wa
shahada ya uuguzi lakini, aliamua kuachana na kasumba ya usomi kama ilivyo kwa
wanawake wengi na kuitazama jamii yake na kutambua inahitaji kitu gani.
“Mateke ni fadhila
ya punda” alisema Bi.Edna na kuongeza, “mimi kama mtanzania na pia
mwanamke msomi sina budi kudumisha utamaduni wangu, elimu yangu isinifanye
kudharau tamaduni yangu na kushusha thamani yangu kama mwanamke”.
Hakika kila mwanamke anapaswa kujifunza katia hili,
ebu tujiulize maswali haya, hii wapi thamani ya mwanamke msomi? kama yeye
mwenyewe ataishusha thamani ya jamii na kudharau utamaduni wake, nani atamuinua
na kusema ameelimika? kuna jambo ambalo wanawake hatujaelewa bado.
Thamani ya mwanamke ni kubwa kulinganisha na kitu
chochote ndani ya jamii, fadhila yake ya usomi kuwa mateke kwa jamii
iliyomuinua sio jambo la kupendeza hata machoni kwa wanawake wengine waliosoma
na hata ambao hawakupata nafasi hiyo ya kusoma.
Kasumba ya usomi wa mwanake kutotaka kufanya kazi
zinazomuhusu hususani zile za ndani, suala la kuhitaji hamsini kwa hamsini na
kusahau majukumu yake muhimu ni jambo lisilokuwa na faida, inatupasa kukumbuka
na kuheshimu jiko la kale pale unapopata jipya.
“Elimu ni jambo zuri na la kimabadiliko kwa mwanamke
kwani ni kwa kupitia elimu hiyo mwanamke anaweza kupambanua mambo yasiyosawa
katika jamii na kujitambua lakini, hulka ya mwanamke isibadilike kutokana tu na
usomi wake”, alisema mwanmke mjasiriamali aliyejitambulisha kwa jina la Bea
Mwombeki.
Kutoa mjadala huu sio kwamba naunga mkono mfumo dume
la hasha naitaji wanawake kutambua thamani yao katika jamii, fadhila ya usomi
isiwe mateke ya kuleta hasara na kupindua jamii na tamaduni kwani, itakuwa sawa
na kurudi katika utawala wa kikoloni na tumeshasherehekea miaka 54 ya uhuru wa
Tanzania.
Mkuu wa maktaba ya hospitali ya KCMC, Moshi
Kilimanjaro, ni moja kati ya mifano bora kwa jamii katika hili, ni mama wa
mtoto mmoja na anaishi pamoja na mume wake Bw. Musa Rajabu, ingawa Bi. Tina
Henry ni msomi na ni mfanyakazi ila hajasahau majukumu yake kama mama.
Bi.Tina anatambua faida za elimu kwa mwanamke na pia
anathamini nafasi yake kwa jamii na familiya yake, anweka bayana kuwa,
mpangilio wa kazi na muda ni muhimu kwa mwanamke, “inawezekana kabisa kuishi
maisha ya dhiki na mume wa ndoa na kumtumikia kama mwanamke kwa kupangilia muda
wa familiya na muda wa kazi, malengo na ratiba ndiyo vitu vinavyomkamilisha
mwanamke msomi” alisema Bi. Tina.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya wanawake
wasomi wamesahau wajibu wao katika jamii na hivyo kujikuta wakidharirika,
kutaka hamsini kwa hamsini sio jambo baya ila, lengo ni nini? kumuinua mwanamke
au kuondoa upekee wake?.
Jambo zuri la kuelewa hapa ni kwamba, mwanamke msomi
ni mwanga kwa jamii na familiya hivyo mwanga huu unatakiwa kutopotosha malengo
na ndoto za wale wanaoufuata mwanga huo bali umulike na kuweka wazi matunda
yaliyobora kwa kujenga na kuweka imara
malengo na ndoto za jamii na familiya.
Makala hii imeandaliwa na Alicia Evance mwanafunzi wa Shule kuu ya Habari na Mawasiliano kwa umma
0 comments:
Post a Comment